Na Mwandishi Wetu
WAKAZI wa jiji la Mwanza na Kanda ya Ziwa wameiomba Kampuni ya Msama Promotions inayoandaa Tamasha la Pasaka na Krismasi kuwapa nafasi ya upendeleo kwa kuwapelekea tamasha katika mkoa huo.
Sababu za kupewa kipaumbele katika Tamasha la Pasaka mwaka huu ni baada ya kulikosa Tamasha la Kirismasi ambalo lilifanyika kwenye mikoa ya Mbeya, Iringa na Songea.
Kwa mujibu wa wakazi hao ambao waliwaomba waandaaji wa matamasha hayo ya injili, Kassim Mtolea mwanafunzi wa Chuo cha SAUT wanamuomba Mkurugenzi wa Kampuni ya Msama Promotions Alex Msama na kamati yake kuwafikiria kwa sababu linashirikisha waimbaji wa Kimataifa.
Mtolea alisema wanamuomba Msama kuwafikiria zaidi kwa sababu miaka yote tangu limeasisiwa limekuwa likianzia jijini Dar es Salaam hivyo ni vyema waandaaji wakabadilika na kulipeleka kwanza Jijini Mwanza.
Aniceth Nyahore ambaye ni mkazi wa Maswa lalieleza kuwa iwapo tamasha hilo litaanzia Mwanza litakutanisha mikoa ya Geita, Shinyanga, Mara na Kagera katika uwanja wa CCM Kirumba na kueneza injili pamoja na burudani.
Nyahore alisema ubora wa Matamasha hayo unatokana na ushiriki wa waimbaji wa Kimataifa wanaotoka nchi za Afrika Kusini, Kenya, Uganda, Rwanda na Uingereza ambao umekuwa ukivutia umati mkubwa wa mashabiki.
Daniel Mkate aliishauri Kamati ya maandalizi kuzingatia kuanza na mkoa wa Mwanza baada ya kulikosa Tamasha la Krismasi lililofanyika mwaka jana huku wakazi hao wakiwa na kiu kubwa.
Sambamba na kuliomba tamasha hilo mkoani humo pia aliishukuru Kamati ya Maandalizi kwa kumleta muimbaji Rebecca Malope ambaye alishiriki tamasha la mwaka juzi.
Aidha Mwenyekiti wa maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama alikiri kupokea maombi haya ambapo alisema ni vigumu kutoa maamuzi maana bado ni mapema mno, lakini aliahidi kuyafanyia kazi.