Na Elizabeth John
STAA wa Bongo fleva nchini, Ally Kiba, amesema kukaa kwake kimya katika ‘game’ sio kwamba ameishiwa, amejaribu kuwaachia wenzie wafanye kazi na kwamba anatumia muda huo kulisoma soko la muziki huo.
Alikiba ni kati ya wasanii ambao walifanya vizuri katika muziki wa kizazi kipya nchini kutokana na uwezo wake wa kuimba na kucheza vizuri anapokuwa jukwaani.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Alikiba alisema wengi wamekuwa wakimsema kwamba ameishiwa mashairi ndio maana amekaa kimya kwa mueda mrefu kitu ambacho sio kweli.
“Niliamua kupumzika kufanya muziki kwa muda mchache nikiwa naendelea na shughuli zangu binafsi, nashangaa kuona maneno maneno ya watu ambao hawana kazi za kufanya, nipo kwenye maandalizi muda mchache tu ntakuja upya na kiushindani zaidi,” alisema.
Alikiba alishawahi kutamba na ngoma zake kama My Everything, Njiwa, Far Away, Mali Yangu, Sinderela na nyinginezo ambazo zilimtambulisha na kufanya vizuri katika tasnia ya muziki huo.