Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuhusu kifo cha Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambaye pia alikuwa Mwanasheria wa chama hicho pamoja na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho. (Picha na Francis Dande)
DAR ES SALAAM, Tanzania
Chama Cha NCCR- Mageuzi kimewataka watanzania kuwa na utulivu wa ndani kufuatia msiba mkubwa wa kuondokewa na Dk. Sengondo Mvungi (61).
Akitoa ratiba ya maziko yake kwa waandishi leo, Mwenyekiti wa chama hicho, James Mbatia alisema wamesikitishwa na kifo cha kiongozi huyo ambaye alikuwa kiungo muhimu.
Mbatia alisema Dk. Mvungi ameacha pengo kubwa ndani ya chama ambalo halitazibika kutokana na kukitumikia kwa moyo mmoja.
Alisema baada kukaa kama chama, familia na serikali, walikubalina na kwamba mwili wake uwasili Novemba 15 mwaka huu toka Afrika Kusini na kupelekwa moja kwa moja katika Hospitali ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Lugalo ambako itahifadhiwa.
Novemba 16 mwaka huu, mwili huo utapelekwa katika Kanisa la Mtakatifu Joseph, Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam saa 3:00 asubuhi hadi 6:00 mchana kwa ajili ya ibada ya kumwombea.
Mbatia alisema baada ya ibada, mwili huo utapelekwa katika Viwanja vya Karimjee kwa ajili ya watu mbalimbali kutoa heshima ya mwisho kuanzia saa 6:30 mchana hadi 10: 00 jioni.
Baada ya hatua hiyo, mwili huo utapelekwa nyumbani kwake Kibamba kupumzishwa ili siku ya Jumapili Novemba 17 uweze kusafirishwa kijijini kwao Kisangara – Mwanga mkoani Kilimanjaro kwa ajili maziko yatakayofanyika Novemba 18 mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Rais Jakaya Kikwete na mkewe Salma jana walikuwa miongoni mwa waombolezaji waliofika nyumbani kwa marehemu Dk. Mvungi kwa ajili ya kuhani.
Rais Kikwete walifika nyumbani hapo saa 6:00 mchana ambapo alipata fursa ya kumpa pole mke wa marehemu, Anna Mvungi, wanafamilia na wananchi waliofika katika msiba huo.
Pia viongozi kadhaa wa serikali, siasa, wanasheria na wananchi wengine walifika nyumbani hapo kuomboleza msiba huo.
Akizungumzia namna alivyomfahamu marehemu, Profesa Kabudi alisema alikuwa ni mtu mzuri asiye mnafiki na aliweza kusimamia kile alichokiamini.
“Dk. Mvungi alikuwa mean disk mwenzangu katika gazeti la Mzalendo pia alikuwa mshehereshaji (MC) wa harusi yangu huku Balozi Costa Mahalu akiwa dereva wa gari la harusi yangu,” alisema.
Naibu Waziri wa Sheria na Katiba, Angela Kairuki, alisema Dk.Mvungi alikuwa ni gwiji la sheria nchini ambaye aliitumia taaluma yake kusaidia wenye mahitaji ya kisheria.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Bagamoyo, Profesa Mahalu alisema amesikitishwa na kifo hicho kwani Dk. Mvungi alikuwa ni mdogo wake kiumri na kwamba kwa pamoja ndiyo walioanzisha wazo la kuanzisha chuo hicho.
Wakati huo huo Chama cha Mapinduzi (CCM) kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Abdulrahaman Kinana kimeeleza kusikitishwa na taarifa ya kifo hicho.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, Kinana alisema kwa niaba ya CCM anatoa pole kwa wanafamilia, Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na Uongozi wa NCCR-Mageuzi.