Quantcast
Channel: HABARI MSETO BLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 19659

LOWASSA APATA KURA 158 MAGUFULI 30 KATIKA KURA ZA MAONI ZILIZOPIGWA NA WANANCHI

$
0
0
Mfanyabiashara wa Kariakoo jijini Dar es Salaam, Ismail Mohamed akisimamia zoezi la kupiga kura za maoni zilizopigwa na wananchi katika maeneo tofauti ambapo mgombea wa  Urasi wa Ukawa kupitia Chadema, Lowassa alipata kura 158 na mgombea wa CCM, John Magufuli alipata kura 30 katika kura zilizopigwa katika maeneo Kariakoo.
 Wananchi wakipiga kura za maoni katika eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam leo ambapo upigaji wa kura ulianza majira ya saa nne mpaka saa kumi jioni.
Akinamama nao walijitokeza katika upigaji wa kura za maoni.
 Kura zikipigwa.
 Mtu mwenye ulemavu wa miguu akipiga kura ya maoni leo.
 Zoezi la kupiga kura likiendelea.
 Ismail Mohamaed (kushoto) akionyesha kura zilizopigwa leo za kumchagua Rais.
Kura zikihesabiwa.

Lowassa ‘kidedea’

*Apata ushindi wa kura za maoni za wananchi

* Ni hasira kutokana na ripoti ya Twaweza
  
xxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxxx

MATOKEO ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Twaweza yameamsha ‘hasira’ za wananchi na kusababisha mivutano ambayo ilimalizika kwa wahusika kupiga kura zao za maoni kuhusu nani anayepewa nafasi kubwa ya kuibuka mshindi kwenye kinyang’anyiro cha urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Ripoti ya Twaweza iliyotolewa hadharani juzi, inaonyesha mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, atapata asilimia 65 na mgombea wa Chadema, Edward Lowassa apata asilimia 25.

Jijini Dar es Salaam, utafiti huo ulizua mjadala mkubwa tangu juzi jioni, huku baadhi ya wakazi wake wakiamua kupiga kura za maoni ambazo zilimuwezesha Lowassa kuibuka kidedea.

Wakazi hao kwa nyakati na maeneo tofauti tofauti waliendesha kura hizo huku wakijinasibu kuwa mchakato wao ni wa uhakika na kwamba ni kiboko ya Twaweza na CCM, kwa kuwa hauna hila wala goli la mkono.

Wananchi hao wanaungana na wasomi pamoja na wanaharakati ambao juzi waliuponda utafiti huo wakisema kuwa umedhalilisha wana taaluma na kwamba ulikuwa na ajenda ya kumbeba Dk. Magufuli.

Profesa Gaudence Mpangala wa Chuo Kikuu cha Ruaha (Ruco) alisema hata kama Dk. Magufuli anaongoza katika kura hizo, haiwezekani kuwapo tofauti kubwa kiasi hicho.

Msomi huyo alifanya rejea ya utafiti wa Twaweza wa Novemba mwaka jana wakati Lowassa akiwa CCM kwamba alimuacha mbali Magufuli, hivyo alihoji iweje leo mgombea huyo aachwe kwa tofauti ya asilimia 40?
Kadhalika usahihi wa taarifa ya Twaweza unatia shaka kutokana na mkanganyiko katika Takwimu zilizotumika kufikia hitimisho husika.

Mathalani, sehemu ya taarifa hiyo inawataja watu sita kati ya kumi waliosema wataichagua CCM kwa urais, kuwa ni sawa na asilimia 66, badala ya asilimia 60.  Ubunge (60%) na udiwani (60%).

Kura za wananchi

Jana katika mitaa ya Soko la Kariakoo, Mtaa
wa Kongo, Uhuru na Mchikichini, wafanyabiashara wa eneo hilo, wateja wao na wapita njia walipiga kura za wazi.

Mfanyabiashara, Ismail Mohamed na wenzake walibeba maboksi mawili yenye majina ya wagombea hao kisha kuyapitisha kila mtaa wakikusanya kura. Maboksi hayo moja lilikuwa na jina la Lowassa na jingine, Dk. Magufuli.

Shughuli hiyo ilianza saa 4 asubuhi ambapo kulikuwa na karatasi ya manila yenye rangi ya njano na peni, kila aliyekutana naye aliombwa aandike jina la mgombea anayempenda.

“Tumefanya hivi kutokana na msuguano ulioibuka kwenye kijiwe chetu kuhusu utafiti wa Twaweza, ambapo tukaona ni busara kufanya hivi ili tujue haki ipo wapi,” alisema.

Mohamed aliyekuwa akisindikizwa na mamia ya wafanyabiashara wenzake, alizunguka katika viunga vya soko hilo hadi saa 10 jioni alipositisha mchakato huo ili kuhesabu kura.

Tanzania Daima lilishuhudia uhesabuji wa kura 188 zilizopigwa hadharani ambapo Lowassa aliibuka na ushindi wa kura 158 huku Magufuli akipata kura 30.

Akitoa maoni yake baada ya matokeo hayo, mfanyabiashara Kulwa Abdallah, alisema wamesikitishwa na utafiti aliodai wa kilaghai uliofanywa na Twaweza.

Hamida Salum yeye alisema ukweli utafahamika siku ya kupiga kura, licha ya kuwa kwa sasa kuna tafiti za uzushi ambazo zinatolewa.

Katika Soko la Kisutu, nako hali haikuwa shwari baada ya kuibuka mzozo ulioamuliwa kwa kupiga kura ya kunyoosha vidole ili kujua nani anapendwa zaidi kati ya Magufuli na Lowassa.
Utata huo uliibuka asubuhi ambapo kati ya watu 40 waliokusanyika eneo hilo, waliomuunga mkono Lowassa walikuwa 33 na Magufuli alichaguliwa na watu saba.

Katika Mtaa wa Mkwepu uliopo Posta, juzi usiku baadhi ya wanywaji wa pombe waliamua kupiga kura baada ya kusikia taarifa ya habari kwenye moja ya kituo cha runinga kikieleza kuhusu utafiti huo wa Twaweza.

Raphael Kessy, muuzaji katika moja ya baa za mtaa huo aliamua kumaliza kelele kwa kugawa karatasi na kuwataka waliokuwa wakibishana wapige kura ili kukata mzizi wa fitina.

“Hapa mpo 21, nimewahesabu, hebu tuache kelele tupige kura ili tujue hao Twaweza ni waongo au wamesema kweli… nakupa karatasi andika Lowassa au Magufuli,” alisema Raphael na kuanza kugawa karatasi za kupigia kura.

Wanywaji hao walipiga kura na matokeo yake Lowassa aliongoza kwa kura 12; Magufuli akiambulia kura saba huku kura mbili zikiharibika.

Mkoani Dodoma baadhi ya wakazi wake walinusurika kupigana ngumi kwenye meza ya magazeti kutokana na ubishi wa matokeo ya utafiti huo.

Mmoja wa wananchi hao ambaye jina lake halikujulikana alisema ni vizuri utafiti ufanyike kwenye vijiwe, stendi na sehemu mbalimbali ili kupata matokeo ya kweli.

“Utafiti gani umefanywa, mbona hatujawaona waje hapa, sasa hivi tupo wangapi hapa, tupo zaidi ya 20, angalia wanaoshabikia CCM ni watatu hapo unaweza kusema nini?
Utafiti huo ni wa kwanza kutolewa tangu kufunguliwa kwa pazia la kampeni za vyama vyote vinavyoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, 2015. Chanzo cha Habari Gazeti la Tanzania Daima Septemba 24

Viewing all articles
Browse latest Browse all 19659

Trending Articles