Na Mwandishi Wetu
MKUGENZI wa Kituo cha Kulelea Watoto Yatima na Wasiona (Chakuwama), Hassan Hamis, ameishauri jamii kujikita zaidi katika kuwasidia watoto yatima ili kuwaepusha na ukosefu wa maadili pindi watakapokuwa wakubwa.
Hamisi alisema hayo wakati kituo hicho kilichoko Sinza wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam, kilipopokea msaada wa vyakula na vifaa mbalimbali vya shule ikiwa ni msaada uliyotolewa na Shirika la Umeme nchini (Tanesco).
Alisema, kama watoto hao wataachwa bila msaada wowote basi jamii itambue kuwa huenda taifa likapoteza viongozi bora na kusababisha matatizo makubwa kwa watoto hao.
Hamisi, alisema kwa kulitambua hilo ndio maana imeamua kuwakusanya watoto hao kwa kuwaweka pamoja na kuwapatia msaada mbalimbali ikiwemo elimu.
“Kituo chetu kina watoto 60 na tunawapatia huduma ya elimu ambayo ni muhimu katika taifa letu kwani tunaimani kuwa hapa tutazalisha wataalamu na viongozi bora wa kesho,”alisema.
Pamoja na changamoto zinazokikabili kituo hicho bado hawajakata tamaa hivyo wanashukuru inapotokea wadau wanapowapatia msaada kama ililivyofanya Tanesco.
“Nashauri wadau wawasaidie watoto hawa na isiwe katika kituo hiki tu bali katika vituo vyote vinavyojitolea kuwalea itakuwa tumewaondolea matatizo yanayoweza kuwakabili watoto hao,”alisema Hamisi.
Kaimu Mkurugenzi wa Tanesco, Dekland Mhaiki alisema walifika katika kituo hicho ili kujionea maendeleo ya watoto hao pamoja na changamoto zinazowakabili wanaamini watakaporudi tena watakuwa na ufumbuzi katika kile walichokiona.
“Nimefarijika kuona maendeleo ya watoto hawa katika kituo hiki na tumewapatia vifaa vya shule na vyakula vya aina mbalimbali kama sehemu ya mgawo wetu,”alisema Mhaiki.