Na Mwandishi Wetu
BAADHI ya wakazi wa eneo la Mloganzila wilayani Kisarawe Mkoa wa Pwani wapatao 64 wamesema hawako tayari kupitisha ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (MUHAS), hadi watakapolipwa fidia zao.
Kauli ya wakazi hao inakuja siku chache baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Said Meck Sadick, kudai kuwa mgogoro wa wakazi hao wakuzuia ujenzi wa kupitisha miundombinu ya umeme, maji na barabara kuwa umekwisha na wamekubali kuyatoa maeneo yao.
Wakizungumza kwanyakati tofauti na Tanzania Daima jijini Dar es Salaam, wakazi hao walisema wanapinga kauli ya mkuu wa mkoa kwamba eneo hilo lina mgogoro, hiyo sio kweli na ukweli ni kwamba wananchi hao wanasubiri walipwe fidia zao ambazo hawajalipwa, zaidi ya ushawishi wakutakiwa kuondoka kabla ya malipo hayo.
Wakazi hao waliozuia ujenzi huo kwa madai ya kutolipwa fidia na baadhi yao kwenda mahakamani walisema hakuna makubaliano yaliofikiwa kati yao na mkuu wa mkoa wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo hilo la mradi Machi 11 mwaka huu na kwamba aache kuoa taarifa za uongo kwa Rais Jakaya kuwa wananchi hao wamubali kuachia maneo yao.
Walisema hawapingi mradi huo bali kinachowachelewesha kuondoka katika maeneo hayo kunachangiwa na serikali yenyewe kutokana na kushindwa kwake kutekeleza ulipaji wa fidia kwa wakazi hao ambao hawana mgogoro na serikali yao.
Wakazi hao, walisema msimamo wao wakutoondoka katika maeneo yao utaendelea kubaki pale pale hadi hapo serikali itakapotekeleza ahadi zake kulipa kwa vitendo na si vinginevyo.
Wananchi hao walisema kuwa wao ni Watanzania ambao wanazo haki zao na ni lazima ziheshimiwe hata kama hawana majina makubwa, viongozi wasipende kutoa amri za vitisho katika kutatua masuala ambayo yangeweza kumalizwa kirahisi bila ya wakati mwingene kufikishana mahakamani
“Siyo kweli kuwa tumefikia muafaka baada ya mazungumzo baina yetu na mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Mecki Sadiki aliyetembelea eneo la mradi, kwa tulimshangaa kuja akiwa pekeeake bila ya kuwa na viongozi wnzake wa mkoa wa Pwani kwa sababu eneo hili ni la Mkoa wa Pwani,”alisema mmoja wa wakazi hao.
Akizungumzia zira ya ya mkuu wa mkoa, Fredy Masondele, ambaye eneo lake ndiko kunakotakiwa kupitishwa umeme mkubwa kwenda kwenye eneo linakojengwa mradi huo, alishangaa kuona ujumbe huo ukiandamana na madifenda zaidi ya manne yakiwa na akari waliokuwa na silaha pamoja na mabomu ya kutoa machozi.
“Niliwapeleka kwenye eneo la nyumba yangu na kuwaeleza kuwa mimi ni muathirika sina mgogoro na serikali ninachotaka ni kulipwa fidia ili ni weze kurudi kwetu Musoma,”alisema Masondole.
Alisema baada ya mazungumzo mkuu wa mkoa akamuahidi kuwa wakati akisubiri fidia serikali itampangishia nyumba ili kupisha mpango wa kupitisha umeme ambao unahitajika kwa haraka uendelee haraka.
Masondole alisema hata kabla ya kupangishiwa nyumba hiyo, alishangaa kuwaona Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kufika katika eneo la nyumba yake mwishoni mwa wiki, wakiwa na magari ya polisi wakijihami na silaha, na kusimamisha nguzo hizo kwa nguvu.
Mwenyekiti wa Kijiji hicho, Mohamed Kikonyo, alisema haelewi ni utaratibu gani ulitumika kwa viongozi hao wa mkoa wa Dar es Salaam kufika katika eneo hilo bila ya ofisi yake kupewa taarifa.
“Huu ni udhaifu wa baadhi ya viongozi wa ngazi za juu kushindwa kutambua viongozi ngazi za chini, bado wanapaswa kutuheshimu kwa kuwa tumechaguliwa na tupo karibu zaidi na jamii,”alisema Kikonyo.
Alimshangaa mkuu wa mkoa huyo, pale alipojaribu kukutana na mkazi mmoja na kumuahidi malipo ya fidia wakati eneo hilo linawananchi zaidi ya 64, ambao hadi sasa hawajalipwa haki zao hali hiyo inawafanya baadhi ya wananchi kutilia shaka mpango mzima ulipwaji wa fidia, kitendo kitakachofanya mafanikio ya mradi huo kukumbana na changamoto zaidi.
Wakati akiwa katika eneo la mradi juma lililopita Meck Sadik alisma mkoa kwa kushirikiana na Shirika la Ugavi wa Umeme nchini (Tanesco), Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dar es salaam (Dawasco), na Wakala wa Barabara Nchini (Tanroad), walikaa pamoja ili kupata ufumbuzi wa mgogoro huo ili kuruhusu kuanza kwa ujenzi wa mradi huo haraka iwezekanavyo.
“Tumekua na mazungumzo na wenzetu hawa na leo tulikua na kikao cha pamoja ili tupate ufumbuzi wa suala hili na tayari wakazi hawa wawili ambao nyumba zao ziko kwenye eneo yatakapopita mabomba ya maji, nguzo za Umeme na Barabara tumezungumza nao na tayari wamekubali na kesho ujenzi unaendelea” alisema Sadik.
Akiwa katika eneo la ujenzi wa mradi huo unaojengwa na Kampuni ya Kolon Global Corporation kutoka Korea, Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Sadiki, alimesema kuwa mradi huo kwa muda umeshindwa kuendelea kutokana na kukosekana kwa maji,umeme na miundombinu ya barabara.