Na Elizabeth John
BAADA ya kutamba na ngoma yake ya ‘Kama Jana’, msanii wa muziki wa kizazi kipya nchini, Juma Kassim Nature ‘Sir Nature’ amekana kumdisi msanii mwenzie, Naseeb Abdul ‘Diamond’ kufuatia mashairi yaliyosimama katika wimbo huo.
Wadau mbalimbali wa muziki huo, wamemshutumu Nature kwa kumuimba Diamond katika wimbo huo na kusema kwamba ni wivu wa kimaendeleo.
Mkazi wa Mwananyamala, Flora Linus, alisema katika wimbo huo, Nature anamtaja Diamond kwa kumkashifu na kusema kwamba kaja jana katika ‘game’ na kwamba hawezi kuwasumbua wakongwe.
“Kiukweli sio vizuri, msanii unapoamua kuingia katika fani unatakiwa ujipange unapokuja ovyo lazima uangukie pua na ukifunikwa na wenzio unaanza kuwaponda kiukweli sio vizuri ni wengi wenye tabia kama hiyo,” alisema.
Alipotafutwa Nature kulizungumzia hilo alisema kuwa, kwa mtu ambaye hajausikiliza vizuri wimbo huo atasema kamsema Diamond lakini katika wimbo huo kamuimba mwanadada ambaye msanii chipukizi anaitwa ‘Dada Mondi’.
“Hamna nilipomdisi Diamond, watu wanapenda kuongea vitu wasivyo na uhakika navyo, pale katajwa mtu mwingine kabisa anaitwa Dada Mondi na anakaa mitaa ya kwetu bado hajatoka halafu anapenda sifa,” alisema.
Nature ni kati ya wakongwe wa muziki huo ambao bado wanaendelea kutamba katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva kutokana na uwezo wa kutunga mashairi na kuwateka mashabiki wa muziki huo.