Na Elizabeth John
MWANADADA anayetamba katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya nchini, Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’ au ‘Komando’ amesema anataka kuliweka jina lake la Komando kuwa na maana kwa kuanza kujifunza kareti.
Kupitia ukurasa wake wa facebook, Jide ameweka picha mbalimbali ambazo zinamuonesha akiwa katika mazoezi ya mchezo huo na kuandika kwamba anataka kuingia katika mchezo huo.
Alisema, ameona aongeze kipaji kingine na kwamba mchezo huo alikuwa anaupenda tangu akiwa mdogo na ndio sababu ya kukubali kupachikwa jina hilo la ‘Komando’.
“Mchezo huu naupenda sana na ndio maana nimeamua kuanza kujifunza, nataka kuwaonesha mashabiki wangu halisi ya jina komando kwamba lina maana gani,” aliandika Jide.
Msanii huyo ni kati ya wakongwe wa muziki huo ambao wanafanya vizuri katika tasnia ya muziki wa kizazi kipya kutokana na ubora wa mashairi ambayo yanasimama katika nyimbo zake.
Jide kwasasa anatamba na kazi yake mpya ya ‘Historia’, ambayo inafanya vizuri katika vituo mbalimbali vya redio na televisheni kutokana na ubora wa mashairi yaliyopo ndani yake.