Quantcast
Channel: HABARI MSETO BLOG
Viewing all articles
Browse latest Browse all 19659

Article 2

$
0
0
Edna Kiplagat: Nakuja Uhuru Marathon

Na Mwandishi Wetu

BINGWA wa dunia wa mbio za marathon, Edna Ngeringwony Kiplagat wa Kenya amejitokeza kushiriki zile za Uhuru Marathon zinazotarajiwa kufanyika jijini Dar ers Salaam Desemba 8, mwaka huu.
Katibu wa Kamati ya Uhuru Marathon, Innocent Melleck ndiye aliyethibitisha hilo na kusema, wamefarijika kwa kiasi kikubwa kwa Edna mwenye sifa lukuki katika mbio za marathon kujitokeza kushiriki.
“Kwetu tumefarijika mno kutokana na ushiriki wa Edna, kwani ni mwanariadha wa kimataifa mwenye rekodi nyingi za kuvutia na hasa hii ya ubingwa wa dunia kwa upande wa wanawake,” alisema.
Edna,34, alitwaa ubingwa wa dunia kwa upande wa marathon mwaka 2011 katika mashindano yaliyofanyika Daegu, Korea Kusini na akafanya hivyo tena mwaka huu katika mashindano ya dunia yaliyofanyika Moscow, Urusi.
Pia alishinda katika mbio za Los Angeles Marathon na New York Marathon zilizofanyika mwaka 2010 na muda bora zaidi kupata kuuweka katika mbio hizo ni wa saa 2:19:50 katika mbio za London Marathon mwaka jana.
Pia ametwaa medali mbalimbali katika mashindano ya vijana wakati anaanza kukimbia mwaka 1996, pale alipoonyesha uwezo wake katika mashindano ya dunia kwa vijana.
Edna ni nani?
Edna Ngeringwony Kiplagat alizaliwa Septemba 15, 1979 na ni mkimbiaji wa mbio ndefu mwenye jina kubwa duniani, hasa baada ya kufanikiwa kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia yaliyofanyika Daegu mwaka 2011 na Moscow mwaka huu.
Alianza kujitengenezea jina pale alipofanya vyema katika mashindano ya Los Angeles na New York City Marathons mwaka 2010.
Katika mbio za mita 3000, Kiplagat pia alishawahi kufanya kweli kwa kushinda medali ya shaba katika Mashindano ya Dunia ya Vijana yaliyofanyika mwaka 1996 na kufanya hivyo mwaka 1998 kwa kutwaa medali ya fedha.
Rekodi yake bora zaidi ya kukimbia katika mita 3000 ni muda wa dakika 8:53.06 ambayo aliiweka mwaka 1996 katika mashindano hayo ya dunia kwa vijana wakati huo akiwa na miaka 16 tu.
Katika Mbio za Nyika za Dunia zilizofanyika mwaka 2006, Kiplagat alimaliza katika nafasi ya 13 na akaja kuweka muda mzuri wa mita 5000 mwaka huo wa dakika 15:57.3 katika mashindano yaliyofanyika Nairobi na baadaye katika nusu marathon akaweka muda wa saa 1:09:32.
Juni 2007 alikimbia mbio za mita 10,000 kwa muda wa dakika 33:27.0 mashindano yaliyofanyika Nairobi, ambapo pia mwaka 2006 alishinda mashindano ya Virginia Beach Rock 'n' Roll Half Marathon, huku 2007 akishinda yale ya Lilac Bloomsday Run na Bay to Breakers yaliyofanyika San Francisco.
Kiplagat alishinda mashindano ya Los Angeles Marathon mwaka 2010 na baadaye akaenda kufanya kweli New York City Marathon na mara mbili aliwashinda wapinzani wake wakubwa Shalane Flanagan wa Marekani na Mary Keitany wa Kenya, ambapo wapinzani wake hao walishika nafasi ya pili na tatu.
Katika mashindano ya riadha ya dunia ya mwaka 2011, Kiplagat ‘alipiga’ muda wa saa 2:28:43 lakini ilikuwa ngumu kwake kwani ikiwa bado kilomita 5 alionekana kushindwa, lakini mshirika mwenzake Sharon Cherop aliamua kusimama na kumsaidia kuhakikisha anamaliza mbio hizo.
Kiplagat, Cherop na Priscah Jeptoo walifanikiwa kutwaa medali zote tatu za juu na kuifanya Kenya kuwa taifa la kwanza kutwaa medali tatu katika mashindano makubwa kama hayo. Baadaye alishiriki Montferland Run huku akiwa na maumivu lakini akamaliza wa pili nyuma ya Abebech Afework.
Mwanariadha huyu anafundishwa na mumewe Gilbert Koech, kitu kinachodaiwa kumfanya kuwa bora zaidi kila siku.
Uhuru Marathon
Mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema wamefurahishwa na ujio wa mwanariadha huyo na kusema wazo kubwa la kuanzisha mbio hizo ilikuwa ni kutaka kuwakumbusha Watanzania kuuenzi umoja, amani, mshikamano ulipo pamoja na uhuru wetu.
“Sisi kama vijana tukaona kuna haja ya kufanya kitu cha kuwakumbusha Watanzania wenzetu kwani tunatakiwa kudumisha urithi wa amani, mshikamano na uhuru wetu tulioachiwa na mababu zetu,” alisema.
Melleck alisema mbali na mbio hizo kufanyika siku hiyo, pia kutakuwa na tamasha kubwa la burudani litakalofanyika katika Viwanja vya Leaders vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam ikiwa ni mkesha wa kusubiri siku ya Uhuru.
Melleck, anasema lengo la mbio hizo ni kuwakumbusha Watanzania umuhimu wa kukumbuka, kuzingatia na kuuenzi urithi waliaochiwa na viongozi waliopigania uhuru wa nchi.
Anasema, urithi huo ambao utakuwa ukikumbukwa kila mwaka kupitia mbio hizo, ni upendo, mshikamano, umoja na amani iliyopo.
Mratibu huyo anasema, ana imani mbio hizo zitajizolea umaarufu mkubwa, kutokana na jinsi zitakavyoteka hisia za watu mbalimbali, wakiwemo wanamichezo.
Katika mbio hizo, zitakazowashirikisha watu wa kada mbalimbali, zitakuwepo pia mbio za kilomita 3, kilomita 5, Half Marathon kilomita 21 pamoja na Full Marathon yenyewe kilomita 42.
Mratibu huyo anasema mbio za kilomita 3 zitakuwa maalumu kwa ajili ya viongozi wa kada mbalimbali, wakiwemo pia wale wa dini na zile za kilomita 5 pia zitakuwa za kuchangia kwa ajili ya watu wa mahitaji ya aina mbalimbali.
Tusubiri kuona ushindani halisi kutoka kwa bingwa kama Edna Kiplagat katika Uhuru Marathon.
WASIFU
Jina: Edna Kiplagat
Kuzaliwa: Novemba 15, 1979
Nchi: Kenya
Urefu: Futi 5 inchi 4
Uzito: Kilo 50
Mchezo: Riadha -MarathonAthletics
Rekodi:    Dhahabu -2011 Daegu Marathon
Dhahabu- 2013 Moscow Marathon
Mashindano ya Vijana
Shaba- 1996 Sydney mita 3000
Fedha- 1998 Annecy mita3000

Viewing all articles
Browse latest Browse all 19659

Trending Articles



<script src="https://jsc.adskeeper.com/r/s/rssing.com.1596347.js" async> </script>