Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye ameteua Kamati Maalum ya Hamasa kuelekea Mashindano ya AFCON chini ya umri wa miaka 17 yatakayofanyika mwezi May 2017 nchini Gabon ambapo Tanzania inawakilishwa na Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Vijana (Serengeti Boys).
Kamati hiyo ya watu kumi(10) itaongozwa na Mwenyekiti Charles Hillary kutoka Azam Tv na Katibu wake Selestine Mwesigwaambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na wajumbe wa kamati hiyo ni Dkt Hassan Abass Mkurugenzi Idara ya Habari MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Ruge Mutahaba Mkurugenzi wa Vipindi na Uzalishaji kutoka Clouds Media Group.
Wengine ni Hoyce Temu Mrembo wa Tanzania mwaka 1999, Maulid Kitenge Mtangazaji kutoka EFM, Beatrice Singano Mkurugenzi wa Mawasiliano Airtel Tanzania, Erick Shigongo Mkurugenzi wa Global Publishers na wasanii wa muziki wa kizazi kipya Ali Kiba na Naseeb Abdul (Diamond Platinumz).
Lengo kuu la Kamati hii ni kuhamasisha watanzania kuiunga mkono Timu ya Serengeti Boys na juhudi za Serikali katika kuhakikisha wanarudi na ushindi katika mashindano hayo.
Imetolewa na

Zawadi Msalla
Kaimu Mkuu waKitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo.
28/02/2017