NA KENNETH NGELESI,MBEYA
KUTOKANA na uelewa mdogo wa wananchi juu ya sheria ya makosa ya mtandao na miamala ya kielektroniki kumekuwa na tafsiri hasi kwa wananchi juu ya maudhui ya sheria hizo na kuzifanya kuonekana kandamizi zaidi kitu ambacho ni tofauti na dhana ya sheria hizo.
Kufuatia upotoshaji huo wa sheria ,serikali kwa kupitia wizara ya mawasiliano na sayansi na teknolojia imekuwa ikitoa elimu kwa umma kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali.
Akizungumza katika ufunguzi wa kikao cha sheria za makosa ya mitandao na miamala ya kieletroniki za mwaka 2015 kwa niaba ya Katibu Mkuu wizara ya mawasiliano na sayansi na Teknolojia ,Ofisa Utumishi Mkuu wa Wizara hiyo, Judith Ndaba alisema washiriki wakuu wa kikao hicho ni kutoka mikoa ya Mbeya ,Iringa,Njombe pamoja na Rukwa .
Hata hivyo alisema kuwa mbali na kufanya semina hizo kwa makundi hayo pia wamekuwa wakitoa elimu ya utekelezaji wa sheria hizo kwa njia ya vipindi vya redio na Luninga.
Ndaba alisema kuwa katika kutekeleza hilo wizara imeona ni vema kuanza kujenga uelewa kwa jeshi la polisi ,waendesha mashitaka,wachunguzi, wapelelezi,Mahakimu,Majaji kuhusu sheria hizo kwasababu ndo wadau wakubwa wa utekelezaji wa sheria hizo.
“Mtakumbuka kuwa namo April mosi 2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha sheria ya makosa ya mtandao ya mwaka 2015 na sheria miamala ya kieletroniki sheria hizi ni muhimu ni vema jamii ikajua umuhimu wa sheria hizi hasa nyakati hizi ambapo matukio ya uharifu yamekuwa yakiongezeka na hakukuwa na sheria mahususi na kukabiliana na matukio hayo’alisema Ndaba.
Akizungumzia madhara ya Mitandao ,Mwanasheria toka Wizara ya Mawasiliano,Eunice Masigati alisema kuwa watu mil.556 wanaathirika kwa mwaka wakati kwa siku ni watu mil.5 na kwa sekunde ni laki Tano wanaathirika kutokana na matumizi mabaya ya mitandao huku asilimia kubwa ikiwa ni vijana.
Hata hivyo Masigati alisema kuwa mbali na kuwepo na idadi kubwa ya vijana kuathirika kutokana na matumizi mabaya ya mitandao lakini pia kumekuwepo na matukio ya wizi wa fedha kwa kutumia miamala ambapo kwa mwaka zaidi ya Dolla Bil.114 zinaibwa kwa mwaka.
Kwa upande wake mshiriki wa semina hiyo ,Hakimu Mkazi wilaya ya Nkasi ,Lilian Rutehangwa alisema wao kama watoaji wa haki kwa wananchi kupitia elimu hiyo watahakikisha wanatenda haki sawa licha ya kuwa katika eneo lake la kazi hajapata kesi zinazohusiana na masuala ya wizi ama uharifu wa mitandao.