Gari la Mgombea Ubunge jimbo la Mbeya Mjini Joseph Mbilinyi Sugu likiwa kituo cha Polisi kati jijini Mbeya mara baada ya kushambuliwa kwa mawe. Picha Kenneth Ngelesi Mbeya. |
Sugu akiwa kituo cha Polisi na wafuasi wake. |
Na Emanuel Kahema, Mbeya
MGOMBEA ubunge kupitia chadema jimbo la Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi leo amejikuta katika wakati mgumu baada ya msafara wake kushambuliwa na watu wasiofahamika na watu wawili wamejeruhiwa akiwemo dereva aliyekuwa akimuendesha mgombea huyo.
Tukio hilo la kushambuliwa kwa msafara huo, limetokea majira ya saa 11 za jioni katika eneo la barabarani lililopo katika Kata ya Ghana mtaa wa Mbata jijini hapa ambapo inasemekana mgombea huyo alikuwa katika harakati za kampeni kuomba kura kwa wananchi wa Iziwa ambapo mgombea huyo alikuwa ndani ya gari yake yenye namba za usajili T161 CPP Toyota Land Cruser VX .
Kutokana na hali hiyo mgombea huyo wa ubunge mbeya mjini kwa tiketi ya Chadema alilazimika kukatisha zoezi lake la kuongea na wakazi wa Kata ya Iziwa iliyopo Jijini Mbeya kwa muda, kutokana na kulazimika kuripoti katika kituo cha polisi kwa ajili ya kutoa maelezo.
Mgombea huyo ilimlazimu kufika kituoni na kuchukuliwa maelezo na baada ya hapo aliruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kisiasa lakini gari yake yenye namba za usajili T161 CPP aliyokuwa akiitumia katika kampeni zake ikibaki polisi.
Hata hivyo, mgombea huyo alipomaliza kutoa maelezo katika kituo cha polisi cha kati cha Wilaya ya Mbeya, aligoma kuzungumza na vyombo vya habari ambavyo vilikuwa kwenye eneo la tukio na kuwataka wafike katika mkutano kwani ndipo atakapotolea ufafanuzi wa suala hilo hilo.