Ofisa Mtendaji Kata ya Temeke, Elias Wawa akizungumza katika uzinduzi wa awamu ya pili kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake masokoni uliofanyika soko la Temeke Sterio Dar es Salaam jana. Uzinduzi huo upo chini ya mradi wa Mpe Riziki si Matusi 'Acha Lugha Chafu na Udhalilishaji Sokoni' Unaendeshwa na Shirika Equality for Growth (EfG).
Mwenyekiti wa Mtaa wa Matumbi uliopo katika wilaya ya Temeke, Khatibu Lindi, akizungumza katika mkutano huo.
Mkazi wa Chamanzi, Husna Abdallah akielezea udhalilishaji wa jinsia katika masoko.
Wasanii wa kundi la Machozi wakiigiza igizo la ukatili wa jinsia
Maofisa wa EfG wa ndani na nje ya nchi na wadau mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi huo.
Na Dotto Mwaibale
OFISA Mtendaji wa Kata ya Temeke, Elias Wawa amelipongeza Shirika la Equality for Growth (EfG), kwa jitihada zake na kupunguza ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake masokoni.
Wawa alitoa pongezi hizo Dar es Salaam jana, wakati akizungumza na wanahabari katika uzinduzi wa awamu ya pili ya kupinga vitendo vya ukatili wa jinsia dhidi ya wanawake katika Soko la Temeke Sterio.
"Nalipongeza shirika la EfG kwa jitihada zao za kutoa elimu kwa wananchi katika masoko mbalimbali kwani imesaidia kupunguza vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa jinsia masokoni" alisema Wawa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Ofisa Mradi wa Shirika la EfG, Susan Sitta alisema shirika hilo lililosajiriwa Septemba 6, 2015 dhima yake ni kuinua maendeleo ya sekta isiyo rasmi Tanzania, hususani wanawake, kwa kupunguza umaskini kwa njia ya kutoa mafunzo ya sheria na haki za binadamu, kutoa msaada wa kisheria, kuwezesha kuwepo kwa fursa za biashara kwa wanawake na wanaume pamoja na kushawishi utungaji wa sera zinazoinua wanawake na kujenga uwezo sawa kwa wanawake na wanaume.
Sitta alisema shirika hilo linatekeleza mradi unaoitwa Mpe Riziki si Matusi katika masoko sita Wilayani Ilala ambayo ameyataja kuwa ni Feri, Kisutu, Mchikichini, Gezaulole, Tabata Muslimu na Temeke Sterio.
Alisema mradi huo umelenga kuwalinda wanawake katika sekta isiyo rasmi hususani wafanyabiashara masokoni dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Aliongeza kuwa mradi huo pia unaangalia wanawake wafanyabiashara katika masoko ya ya Wilaya ya Ilala na Temeke na kuhakikisha wanafanyabiashara zao katika mazingira huru yasiyo na ukatili wa matusi, kingono, kimwili, kiuchumi na kisiasa.
"Mradi huu zaidi unaangalia na kuhakikisha wanawake wanaheshiwa na kufurahi haki yao ya kiuchumi" alisema Sitta.
Sitta alisema utafiti uliofanywa na shirika hilo juu ya ukatili dhidi ya wanawake masokoni unaonesha asilimia 90.32 ya wanawake katika sekta isiyo rasmi wanafanyiwa ukatili mara kwa mara wa kingono, kimwili na matusi katika maeneo yao ya kazi.
Mkazi wa Chamanzi, Husna Abdallah alisema kufanyiwa viendo vya ukatili wa jinsia kwa wanawake wafanyabiashara masokono kwa upande mwingine kunachangiwa na wanawake wenyewe pale wateja wanapowashika katika miili yao na wao kufurahi jambo hilo bila kuchukua hatua ya kuwakalipia au kuwapeleka kwa uongozi wa soko husika.