NA ZAWADI CHOGOGWE
HOSPITALI ya CCBRT iliopo Msasani jijini Dar es Salaam imefungua kiwanja cha michezo tofauti tofauti ya watoto hospitalini hapo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kiwanja hicho, Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya mbio za mbuzi ‘Dar es Salaam Charity Goat Races’, Karen Stanley alisema kitasaidia katika kuhamasisha afya ya watoto walioko wodini kwa kucheza,kupumzika na kuweza kujumuika na watoto wengine.
Alisema kuwa kuwa CCBRT ilitambua kuna umuhimu mkubwa wa kuboresha kiwanja cha michezo cha watoto kilichokuwa kimechakaa kwa kujenga upya na kuongeza ubora wa kivuli cha kupumzika.
Alisema michezo ina sehemu kubwa katika ratiba za matibabu ya watoto waliopo hospitalini haswa walioko kwa muda mrefu kwa lengo la kuwaondolea mawazo na kuwafanya wawe sehemu ya jamii iliyona afya bora.
“Kulazwa hospitalini si tukio la kawaida na mara nyingi husababisha msongo kwa watoto na familia zao, hivyo kwa kufunguliwa kwa kiwanja hiki kitawajenga watoto kisaikolojia." Alisema na kuongeza kuwa
“Kuwepo kwa eneo hili ambalo watoto wanaweza kucheza,pia husaidia kuwapa muonekano mzuri juu ya muda wao kwa muda wote watakaokuwa hapa hospitalini”
Alisema kwa kupata uwanja huo utawafanya watoto kuweza kumudu baadhi ya matibabu yakiwemo ya upasuaji na magonjwa mengine wakati wakiwa hospitalini.
Stanley alisema kuwa uwanja huo ulianza kujengwa Desemba mwaka jana na kukamilika rasmi mwezi juni mwaka huu kwa udhamini wa mashirika manne ya Irish Aid, Dar es Salaam Goat Races, Corona Society of Tanzania na Familia ya Wetzel.