Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu mdororo wa shilingi. Kulia ni Mkurugenzi wa Masoko, Utafiti na Huduma kwa Wateja, Tully Mwambapa.
Waandishi wa habari wakimsikiliza Dk. Charles Kimei.
Na Mwandishi Wetu
WADAU wa maendeleo nchini hususani wanasiasa, wametakiwa kuacha tabia ya kuishinikiza Benki Kuu ya Tanzania (BOT), kudhibiti mdororo wa shilingi ya Tanzania, kwani si njia sahihi na badala yake waache thamani ya fedha hiyo kukua kulingana mahitaji ya kiuchumi.
Wito huo umetolewa jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Dk. Charles Kimei alipokuwa akizungumzia kushuka kwa thamani ya shilingi ya Tanzania na kusema mashinikizo kutoka kwa wadau hao yanaziathiri taasisi za kifedha, hususani mabenki.
Dk Kimei alisema kuwa shinikizo hilo, linailzimu kwa BOT kuyaminya mabenki, kwani njia nzuri inayotumiwa na taasisi hiyo katika kuzuia anguko hilo na mabadiliko ya fedha za kigeni ni kubana sera za kifedha na kuondoa zaidi shilingi katika mzunguko wake.
“Moja ya athari za kuondoa shilingi katika mzunguko wake ni kupanda kwa riba miongoni mwa watumiaji wa huduma za kibenki, hivyo kupunguza nia ya kukopa waliyonayo wateja wetu na kuathiri mzungunko wetu wa fedha,” alisema Dk. Kimei.
Aliwataka wadau hao, hasa wanasiasa waguswe kwa namna moja ama nyingine na ukuaji huo wa riba kwa Mtanzania wa kawaida ambao unaathiri harakati za maendeleo, na kwamba waelekeza nguvu zao katika hilo ili kupunguza ukali wa maisha na kuleta maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa, thamani ya mabadiliko ya fedha ya kigeni ni muhimu katika ukuaji wa uchumi na kuwataka wadau wa maendeleo kujielekeza katika kuiacha shilingi ipande thamani yenyewe kulingana na taratibu za kiuchumi na sio kwa shinikizo.
Hata hivyo alikiri kuwa wao kama taasisi za fedha nchini wanatambua athari za kushuka kwa thamani ya shilingi ambazo ni pamoja na kupunguza wawekezaji wapya kutoka nje, lakini akaonya kuwa kulazimisha nguvu ya shilingi dhidi ya dola kunalipunguzia taifa nguvu ya ushindani kibiashara katika soko la kimataifa.