Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema (katikati) akiongozana na viongozi wa hospitali ya Agakhan jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake leo katika hospitali hiyo.
NA MWANDISHI WETU
HOSPITALI ya Aga Khan iliyopo jijini Dar es salaam imesema itashirikiana na hospitali ya Temeke iliyopo wilaya ya Temeke kwa ajili ya kuhakikisha afya ya mama na mtoto inaboreshwa.
Hayo yalibainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sophia Mjema wakati ya ziara yake hospitalini hapo kujionea huduma zitolewazo na hospitali hiyo kwa kutumia vifaa vya kisasa.
Mjema alisema kupitia ushirikiano huo Temeke hospitali itapata fursa ya kupeleka wagonjwa wake Agha Khan hasa akina mama na watoto kufanyiwa vipimo vya afya na matibabu bure .
Aidha alisema mbali ya huduma hizo pia watalaamu wa Agha Khan watawasaidia wa Temeke katika kuwapa mafunzo ya namna ya kutumia vifaatiba vya kisasa hivyo kubadilisha na ujuzi.
Katika Ziara hiyo Mjema aliwataka watanzania kuacha kwenda kutibiwa nje ya nchi kwa kuwa hivi sasa kuna hospitali zinazotoa huduma zote ambazo ziliwalazimu watu kwenda nje kutibiwa na aliwashauri watumie hospitali hiyo ambayo ina wataalam wa kutosha hususan kwa magonjwa yaliyoshindikana sambamba na vifaatiba vya kisasa.
Pamoja na mambo mengne, Mjema alitoa shukrani za dhati kwa uongozi wa Aga Khan na kuwataka waendelee na moyo huo ili kutimiza malengo ya milenia katika sekta ya afya.
Kwa upande wake Dk. Jaffer Dharsee wa hospitali ya Aga Khan alisema katika kudumisha ushirikiano itatoa mashine ya CT Scan pamoja na wataalam kwaajili ya hospitali ya Temeke ili kuwarahisishia wakazi wa Wilaya hiyo .
Naye Bertysheba ambaye ni mgonjawa aliyekwenda kupata huduma ya Mionzi ya kansa hospitalini hapoa alisifu huduma zitolewazo na Agha Khan sambamba na kuwatoa hofu wagonjwa wa kansa kutoogopa kutibiwa kwa njia ya mionzi kwani ndiyo inayompa ahueni na anatumia kwa mwaka wa tatu sasa.