Na Mwandishi Wetu
MKALI wa muziki wa Bongo fleva, Omary Nyembo 'Ommy Dimpoz' anatarajia kusambaza albamu yake ya kwanza Februari akiwa na lengo la kuwaburudisha wapenzi wa kazi zake.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Meneja wa Dimpoz, Issa Mbarouk 'Mubenga', alisema kuwa licha ya wasanii wengi kudai kwamba albamu hazina faida wao wamejiandaa kuliteka soko hilo.
Alisema kuwa, katika maktaba yao kuna nyimbo zaidi ya 26 hivyo watachagua ni nyimbo gani ziingie katika albamu hiyo ambayo bado haijapatiwa jina.
Mubenga alisema kuwa, mwaka 2015 ni mwaka ambao wamejipangia kufanya makubwa na kuhakikisha msanii huyo anapaa katika mataifa mbalimbali kutokana na ubora wa kazi ambazo atakuja nazo.
"Kuna biashara zetu ambazo tutakuja nazo kwa mwaka huu kwa lengo la kujipatia fedha na kuwapa vijana ajira, kuna bidhaa kama kofia, tsheti na mambo mengine ambayo yatakuza jina la Dimpoz ndani na nje ya nchi," alisema.
Dimpoz alishawahi kutamba na ngoma zake kama Nai nai, Baadaye, Me and You, Ndagushima, Koi Koi, Tupogo na nyinginezo ambazo zilimtambulisha na kufanya vizuri katika tasnia ya muziki huo.