Na mwandishi wetu, Sikonge
Kundi kubwa la Ng’ombe limevamia eneo la Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA), Ipole wilayani Sikonge mkoani Tabora ikiwa ni muendelezo wa wafugaji kukiuka sheria za uhifadhi.
Taarifa zilizotufikia jana, kutoka kwenye eneo hilo la hifadhi zinasema, kundi la Ng’ombe wanaokadiriwa kufikia 2000 lilionekana kwenye eneo hilo na mkuu wa wilaya ya Sikonge, Hadija Mohammed, amesema mtu mmoja anashikiliwa na polisi kuhusiana na ng’ombe hao.
“Ni kweli matukio ya wafugaji kuingia kwenye maeneo ya hifadhi hutokea na tunamshikilia mtu mmoja baada ya kukutwa na Ng’ombe kwenye eneo hilo jana (juzi).” Alisema DC huyo katika mahojiano ya simu jana.
Alisema, tatizo hilo wanajaribu kukabiliana nalo, na kupinga taarifa kuwa wafugaji waliovamia kwenye hifadhi hiyo wanatoka maeneo ya nje ya wilaya hiyo.
“Siyo kweli hakuna mfugaji yeyote kutoka nje ya wilaya hii na huyu tuliyemkamata ni msukuma wa hapa hapa, hakuna wamasai walioonekana kwenye eneo hilo labda taarifa hizo mlizopewa siyo za kweli.” Alifafanua mkuu huyo wa wilaya.
Hata hivyo mkuu huyo wa wilaya aliomba apatiwe muda zaidi ili afuatilie taarifa hizo polisi kwani hata jina la huyo aliyemtaja kuwa amekamatwa alikuwa bado hajapatiwa.
Naye mwenyekiti wa hifadhi hiyo Nurdin Kasanda alisema tukio hilo lilitokea jana jioni (juzi), majira ya saa 12;45, ambapo askari wa eneo la hifadhi waliokuwa doria walikamata ng’ombe wapatao 172.
Hata hivyo wakati wakijiandaa kuchukua hatua za kisheria kwa kutoa taarifa polisi, kundi la wafugaji lilivamia ofisi ya Hifadhi hiyo na kuwatorosha ng’ombe kwa nguvu.
Akielezea zaidi mkasa huo, mwenyekiti huyo alisema, Desemba mwaka jana ng’ombe 400 walikamatwa kwenye eneo la hifadhi, lakini wafugaji walijikusanya na kuwavamia askari na kuwanyang’anya ng’omb hao.
“Kinachotusikitisha, taarifa za uvamizi huu tuliziripoti polisi na tunaambiwa jalada la kesi yetu ndio kwanza limepelekwa jana (Jumanne), huko Tabora kwa hatua zaidi za kisheria.”. Alilalamika
Mwenyekiti huyo alimtaja kijana aliyekamatwa kwenye vurugu za Jumanne, kuwa ni Luhende Ndege mwenye umri wa miaka 17.