Chama cha Wananchi kimesikitishwa na vitendo vilivyofanywa na wafuasi wa Chama cha Mapinduzi wakiongozwa na Katibu wa Uhamasishaji na Kamanda wa Chipukizi UVCCM Paul Makonda kwa kufanya fujo na kusababisha mdahalo kuvunjika ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwenye Ukumbi wa Hotel ya Blue Pearl, Ubungo jijini Dar es Salaam jana alasiri.
Vijana hao wa Chama cha Mapinduzi ambao walionekana kuwa wameandaliwa maalum kuja kumdhalilisha Waziri Mkuu na Makamo wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (Mstaafu) Mhe Jaji Joseph Warioba Sinde, ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Mpya kwa kumtolea matusi, kumzomea na kuonyesha mabongo ya kashifa na ujumbe wa kuipongeza Katiba Pendekezwa.
Vurugu hizo zilizopelekea mdahalo huo kuvunjika, zilisababisha mapigano ya ngumi na kurushiana viti baina ya vijana hao wa CCM na wananchi wengine walikuja kushiriki mdahalo huo ambao hawakupendezewa na vitendo hivyo, ambavyo ni ukikwaji mkubwa wa haki za binadamu na Katiba ya nchi inayoendelea kutumika.
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 toleo la 2005 Ibara ya 18. Kila mtu- (a) anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake; (b) anayo haki ya kutafuta, kupokea na kutoa habari bila ya kujali mipaka ya nchi; (c) anao uhuru wa kufanya mawasiliano na haki ya kutoingiliwa katika mawasiliano yake; na (d) anayo haiki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia kuhusu masuala muhimu kwa jamii.
Halikadhalika katika Ibara ya 20. (1) Kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine, na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.
CUF – Chama cha Wananchi kama CCM wameamua kuilinda Katiba yao Pendekezwa kwa hali yoyote hata kwa kumwaga damu huku midomo yao ikihubiri AMANI NA UTULIVU, na sisi CUF kwa kushirikiana na Vyama vingine vya siasa vyenye nia njema na wananchi tutayalinda mawazo na matakwa ya Wananchi katika Katiba yao waitakayo kwa hali yoyote wanayoikusudia CCM, “Ngoma watakavyoipiga ndivyo tutakavyoicheza”
CUF – Tunawataarifu jeshi la Polisi, kwa vile ni jukumu lao kulinda usalama wa Raia na inaonesha wameshindwa, Sisi CUF tunachukua dhamana hiyo ya kuilinda midahalo itakayomhusu Jaji Warioba pamoja na Wajumbe wa Tume ya Katiba na Taasisi ya Mwalimu Nyerere kwa nia njema ya kutoa elimu ya Uraia juu ya Katiba Inayopendekezwa. Jaji Warioba ni Kiongozi wa Taifa hili hivyo kwa namna yoyote ile hawezi kudhalilishwa huku CUF kama wadau wa Mambo ya Siasa na Elimu ya Uraia tukiwa kimya.
CUF – Tunalitaka Jeshi la Polisi kuwakamata wahusika wote waliosababisha uvunjifu wa amani na kuhakikisha wanapelekwa katika vyombo vya sheria wakishitakiwa kwa makosa ya jinai.
Imetolewa na Abdul Kambaya
Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma Novemba 3, 2014
Imetolewa na Abdul Kambaya
Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano na Umma Novemba 3, 2014