Na Ferdinand Shayo, Arusha
Ofisa Uhusiano na Huduma kwa wateja ,TANESCO Arusha, Benedict Nkini amesema kuwa wako katika awamu ya pili ya utekelezaji wa mradi huo wa umeme vijijini na kwasasa wanaelekea katika wilaya za Arumeru, Karatu, Monduli na Longido lengo ni kuhakikisha wananchi waishio vijijini wanafikiwa na huduma hiyo muhimu.
Benedict Nkini akizungumza katika mkutano na Wananchi wa Vijiji vya Meserani juu na chini amesema kuwa kwa sasa wako katika hatua ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya mradi huo ili waweze kujiandaa kuunganishwa na huduma hiyo na pia amewataka waepuke vishoka ambao hutumia uelewa mdogo wa wananchi kujinufaisha.
Afisa Masoko wa Tanesco,Adelina Lyakurwa amesema kuwa amewaomba wananchi kutumia fursa hiyo kuunganishiwa umeme huo wa bei nafuu ambao Mtanzania wa hali ya chini anaweza kuumudu ,ambapo Mwanakijiji atatakiwa kuwa na kiasi cha shilingi 32900 ili aweze kuunganishiwa umeme.
“Tunawaunganishia umeme watu wote wenye nyumba za mawe,matofali,mbao kwa hiyo tunawaomba wananchi watoe ushirikiano ili kufanikisha mradi huu,kwa upande wa nyumba za nyasi na makuti kunahitajika ushauri wa kitaalamu kwasababu za kiutaalamu ili kuepuka moto ambao unaweza kutokea kutokana na hitilifu ndogo” Alisema Afisa Masoko.
Kaimu Mkurugenzi wa TANESCO wilaya ya Monduli0, Ramadhani Mkayala amewataka wananchi watafute wakandarasi wazuri waliodhinishwa na shirika ili kuepuka vihatarishi vya moto
Kwa upande wao wananchi wa Wilaya ya Monduli Sophia Mligo wa kijiji cha Miserani na Gasper Lengta wamesema kuwa wameupokea mpango huo vizuri na kuwaomba TANESCO wazidi kufanya ushirikishaji zaidi na wananchi ili uweze kufanikiwa bila vikwazo.
“Kuna wakati tulihisi kuwa serikali imetusahau watu wa vijijini lakini sasa tunafarijika kuona hawa REA na TANESCO wanakuja kutuunganishia umeme na tayari wameanza kuchimba mashimo kwenye kijiji chetu shughuli iliyobaki ni kufukia nguzo ,uhakiki ulishafanyika hapo awali” Alisema Parirong’o Sipitieki ambaye ni Mwenyekiti wa Kijiji cha Ingoikumeni.