NA MWANDISHI WETU
VIONGOZI wa benchi la ufundi la Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ pamoja na madereva wa mabasi ya timu hiyo, wamelikalia kooni Shirikisho la Soka Tanzania, ili liwalipe stahiki zao, licha ya timu kutolewa katika michuano ya Kimataifa.
Stars ilikubali kichapo cha mabao 4-3 kutoka kwa timu ya Taifa ya Msumbiji na kujikuta wakifungashiwa vilago kuwania kushiriki mashindano ya Mataifa ya Afrika maarufu kama AFCON mwakani nchini Morocco.
Katika mchezo wa awali Stars ililazimishwa sare ya mabao 2-2, na baadae mchezo wa marudiano ikakubali kichapo cha mabao 2-1 mchezo uliopigwa nchini Msumbiji, na kuyaaga mashindano hayo.
Habari kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, ziliipasha Tanzania Daima jana kuwa, mpaka sasa kila mtu ndani ya timu hiyo isipokuwa wachezaji analidai Shirikisho zaidi ya mil 2 ikiwa ni pesa ya walipokuwa Maputo pamoja na wakati wakiwa Tukuyu Mbeya kwa ajili ya maandalizi.
“Unajua inasikitisha mno, TFF ndo kwanza mwaka mmoja, wameanza kufanya hivi ikifika miaka minne itakuwaje, maana toka tukiwa Tukuyu kambini, hatujalipwa sisi, na tunafamilia zetu, hata madereva pia nao wanalia njaa tu,”alisema mtoa habari huyo.
Chanzo hicho kilienda mbali zaidi, na kusema kuwa, mpaka sasa familia yake haimuelewi kama kweli hana pesa, licha ya kujitahidi kuieleza hali halisi, kwa kuwa wanatambua TFF inawalipa wawapo ndani na nje ya nchi pia.
“Tena sisi tunavumilia mno lakini, uvumilivu umeanza kutushinda sasa, maana familia hazituelewi kusema kweli, hali ni mbaya, kama mimi naulizwa, kama hauna hela ulienda kufanya nini si bora ungekaa nyumbani ikajulikana moja tu,”alisema na kuongeza kuwa, waliulizia wanaambiwa mpaka kufikia Jumatano ya wiki hii watalipwa.