FAMILIA ya marehemu Elinema Massawe imesema wanajipanga kwenda mahakamani wiki ijayo wakidai kupata uhakika kuwa kifo cha ndugu yao chanzo chake kimetokana na kipigo alichopatiwa na polisi wa kituo cha Mbezi kwa Yusufu.
Akizungumzia kifo hicho jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Godfrey Shoo, alisema wanawashukuru Madaktari wa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa kuweka ukweli hadharani kuhusu kifo cha Massawe.
Alidai kuwa kwenda kwao mahakamani kunatokana na viashiria mbalimbali vilivyoelezwa na Daktari (jina tunalo), aliyefanya upasuaji kwamba marehemu alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa tetenasi uliyotokana na jeraha lilitokana na kupigwa risasi.
“Wakati Daktari anatueleza hivyo askari waliohusika na tukio hilo walikuwepo pia akawauliza kwa nini walimpiga risasa kwa mbele wakati marehemu hakuwaakimbia wakashindwa kujibu mbele yake,”alisema Shoo.
Akitoa ufafanuzi kuhusu uchunguzi wa kidaktari, Shoo, alisema hana nakala ya uchunguzi huo lakini wameahidiwa kuipata kwa ajili ya ushahidi wakati watakapokwenda mahakamani.
“Ndugu yetu amepigwa risasi kwa mbele mguu wa kushoto, ambayo ilitokea kwanyuma na kusambaratisha vibaya mguu huo, ni seme tu tumchoka na maonevu acha tuende mahakamani,”alisema.
Shoo alisema familia hivi sasa inaandaa wanafamilia wanne ambao ndio wanaotarajiwa kwenda kufungua kesi hiyo Mahakani wiki ijayo.
Aliongeza kwa kusema kuwa wanawaomba Watu wa haki za binadamu kujitokeza kwa kuwapatia msaada wa kisheria katika tukio hilo ambalo ni moja ya matukio mengi yanayodaiwa kufanywa na askari nchini.
Akizungumzia maziko ya marehemu huo, alisema jana saa sita mchana waliaga mwili huo, kisha kuusairisha kwenda kwao Machame wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mashi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Cmillius Wambura, alisema kweli mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi wa kidaktari, hivyo kinachosubiriwa ni taarifa rasmi za uchunguzi huo na si vinginevyo.
Marehemu Massawe, alikutwa na mauti hayo baada ya kukamatwa na polisi, wiki moja iliyopita akihusishwa na mtandao wa wizi wa magari, wakampeleka kituoni alikodaiwa kupigwa vikali katika shehemu za mwili wake hadi kifo.