Akiwasilisha Rasimu ya Pili ya Katiba bungeni leo, Jaji Warioba amesema uchambuzi uliofanywa na tume yake umezingatia maoni ya wananchi, historia na hali halisi, na kwamba ili muungano udumu serikali tatu hazikwepeki.
Alisema tume ilitafakari maoni mbalimbali yaliyotolewa na wananachi na makundi, na ilirejea ripoti kadhaa za miaka zaidi ya 20 mfululizo, ikazingatia malalamiko ya Zanzibar na Tanganyika, mgongano wa kikatiba kati ya Katiba ya Zanzibar na ya Muungano, na mengine mengi.
Alisitiza kuwa hata hoja ya kwamba serikali tatu zitadhoofisha muungano si ya kweli, kwani muungano si wa viongozi bali wananchi, na kwamba ongezeko la gharama halitakuwa kubwa sana kama inavyofikiriwa.
“Kwa tathmini ya Tume, muundo wa serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa. Muungano wa serikali mbili waliotuachia waasisi si uliopo sasa. Umebadilishwa mara nyingi, wakati mwingine bila ya kufanya mabadiliko kwenye Katiba. Waasisi walituachia Muungano wa nchi moja yenye Serikali Mbili, na si nchi mbili zenye Serikali Mbili,” alisema.
“Kwa tathmini ya Tume, muundo wa serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa. Muungano wa serikali mbili waliotuachia waasisi si uliopo sasa. Umebadilishwa mara nyingi, wakati mwingine bila ya kufanya mabadiliko kwenye Katiba. Waasisi walituachia Muungano wa nchi moja yenye Serikali Mbili, na si nchi mbili zenye Serikali Mbili,” alisema.
Muundo wa muungano kwa muda mrefu limezua mjadala ndani na nje ya Bunge.
Alisema kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilijadili njia bora ya kupata maoni na kufikia hatua ya kuandaa dodoso ili wananchi wajibu maswali kuhusu mambo mbalimbali kuhusu Katiba.
“Hata hivyo tume iliamua wananchi wasipewe mwongozo ili wawe na uhuru wa kusema chochote wanachokiamini ikiwa ni pamoja na suala la muungano,” alisema.
Alifafanua kuwa wananchi wengi waliotoa maoni kuhusu muungano walijikita kwenye muundo wake kama njia ya kuondoa kero.
“Wananchi waliotoa maoni kuhusu muundo wa muungano kwa Tanzania Bara, asilimia 13 walipendelea serikali moja, serikali mbili asilimia 24 na serikali tatu asilimia 61.
“Kwa Zanzibar asilimia 34 walipendekeza serikali mbili, asilimia 60 walipendekeza serikali ya mkataba na asilimia 0.1 (watu 25) serikali moja,” alisema.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, taasisi nyingi kama vyama vya siasa, asasi za kirai na jumuiya za kidini zilipendekeza muundo wa serikali tatu.
“Kwa mfano, Baraza la Wawakilishi lilipendekeza kuwepo na mamlaka huru ya Zanzibar, mamlaka huru ya Tanganyika na mamlaka ya muungano na iweke wazi maeneo, uwezo, nguvu, utendaji na mipaka ya mamlaka,” alisema.