Mkazi wa kijiji cha Nyamihuu jimbo la Kalenga Bw Jackson Kiswaga kulia akikabidhi msaada wa mifuko 10 ya saruji Bw Aidan Nyato mwenyekiti wa baraza la wazee wa Kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Kidamali jimbo la Kalenga. (Picha na Francis Godwin )
Na Francis Godwin,Iringa
MKAZI wa kijiji cha Nyamihuu aliyekuwa mshindi wa pili katika kinyang'anyiro cha kuwania kuteuliwa kugombea ubunge jimbo la Kalenga kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Bw Jackson Kiswaga ametoa msaada wa saruji mifuko 10 kwa uongozi wa kanisa la kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Kidamali wilaya ya Iringa mkoani hapa huku akiwataka watanzania wenye uwezo kuendelea kuchangia nyumba za ibada kama njia ya kulinda amani yetu.
Huku akimpongeza Rais Dr Jakaya Kikwete kwa kuendelea kuongoza nchini kwa hali ya amani na utulivu kwa kila mtanzania kufanya shughuli zake bila kuwepo kwa vitendo vya uvunjifu wa amani kama zilizo nchi nyingine barani Afrika.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada huo jana Kiswaga alisema kuwa ametoa msaada huo kufuatia maombi ya uongozi wa kanisa hilo kwake na kuwa kama mmoja kati ya waumini wa Kanisa hilo aliguswa na jitihada za waumini hao kutaka kumjengea nyumba mchungaji wao.
Hivyo msaada huo utasaidia kuanza ujenzi wa nyumba hiyo ya mchungaji na kuwa ataendelea kuchangia hatu moja hadi nyingine katika ujenzi huo huku akiwataka waumini wengine wa kanisa hilo a wale ambao si waumini wa kanisa hilo kuendelea kujenga utamaduni wa kuchangia nyumba za ibada ili ziweze kutumika katika kuliombea Taifa amani zaidi .
Alisema iwapo watanzania wataelekeza nguvu zao katika ujenzi wa nyumba za ibada nchi itaendelea kuwa na wananchi wacha Mungu na wasiopenda kuona amani inachezewa .
Kiswaga alisema kusaidia nyumba za ibada mbali ya kumwezesha mchangaji kupokea baraka za Mungu katika shughuli zake ila bado ujenzi huo wa nyumba za ibada utachangia watu wachache ambao hawana mazoea ya kwenda katika nyumba za ibada kama Makanisani na Misikitini kushawishika na kumgeukia Mungu.
"Nyumba za ibada ni sehemu ya baraka hivyo lazima watanzania kuendelea kuchuma baraka kwa kuchangia nyumba za ibada"
Akishukuru kwa msaada huo mwenyekiti wa baraza la wazee kanisani hapo Aidan Nyato alisema walilazimika kumwandikia barua Kiswaga na kumuomba msaada wake kutokana na jitihada mbali mbali ambazo amekuwa akionyesha katika kuwaletea maendeleo wananchi wa kijiji hicho na maeneo mengine .
Alisema hadi sasa bado kanisa hilo linaomba kusaidia msaada wa mbao zaidi ya 100 bati 150 ili kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo ya mchungaji .