Na Bryceson Mathias
MWAKA 2010 Katika Kampeni za U-Rais, U-bunge na U-diwani, Wengi mlitoa ahadi Lukuki kwenye mikutano ya hadhara, na huko vijijini kwa kukosa mahali pa kuandika waliziratibu na kuandika kwenye Mawe! Je mnafahamu 2015 si mbali?
Najua mnafahamu fika, miongoni mwenu mliponea kwenye tundu la sindano baada ya kuwalilia wananchi kwa machozi na kutambaa, huku wengine mkiwapigia magoti hata watoto wadogo; Je mnadhani kwa kutotimiza ahadi zenu mtarudi 2015?.
Ahadi mlizoahidi na kutozitimiza, naapa ndizo zitakazowahukumu na kuwatundika Msalabani; Kibaya zaidi sasa hivi imefikia wananchi wakiwapigia simu kuwaeleza Kero zinazowakabili, bila aibu mnadiriki kusema mna kazi nyingi! Wao Ikifika 2015, waseme kazi nyingi kwako?
Nilifika kijiji kimoja, Mbunge na Diwani walijigamba watajenga Zahanati, wakashangiliwa makofi, akina mama wakasema, kitendawili klichokuwa kinahatarisha maisha yao wakati wa kujifungua na kupoteza watoto! Kimeteguliwa.
Cha ajabu katika taarifa za Halmashauri , Diwani na Mbunge kwa kutumia kigezo cha Siasa kuwa ni Uongo, walitoa taarifa katika Kikao chao kuwa, Zahanati ile iko kwenye Lenta kumbe ni Uongo hata msingi haujaisha.
Baada ya Mwenyekiti wa Kijiji na wananchi kuja juu, iliundwa Tume ya Kamati ya Fedha kukagua Miradi inayosuasua akiwemo Mwenyekiti wa Halmashauri (jina linahifadhiwa), ikabaini Zahanati ile haiko kwenye Lenta, bali hata msingi tu bado haujaisha Saruji imeganda.
Nauliza, huyu Diwani na Mbunge, ambaye hata Wakaguzi wamefika eneo la Mradi, wakabaini fedha zimekombwa na Zahanati haijaisha! Je watu wamrejeshe 2015? La hasha, watatumalizia fuko la fedha na maendeleo yao yatakuwa duni miaka nenda rudi.
Pamoja na kuwa tunawakoromea Madiwani na Wabunge kwa Ahadi walizowaahidi wananchi na wakaziandika kwenye mbao za Mawe, bado nina Hoja na Watendaji wa Rais, Je Mnakumbuka kuikumbusha Serikali kuhusu Ahadi zake?
Kama Rais aliahidi Gari la Wagonjwa mahali, Maji, Umeme, Barabara au kitu chochote cha kuwatendea wananchi kote alikopita nchini kuomba kura,; Je kuna mahali mliandika hivyo kuikumbusha Serikali na Mamlaka husika kutekeleza ahadi hizo?
Kama watendaji hamkuandika popote, mlibaki mnakula Ma-Kuku na Vinywaji Rais akitoa ahadi katika Kampeni 2010, Mwaka 2015 si mbali upo mlangoni, mtamfanya Mgombea U-rais ajaye apate wakati Mgumu kwa aliyoahidi mwenzake, maana watamuonesha ahadi hizo kwenye Mawe waliyoandika!
Ili kumuepushia adha mgombea U-rais ajaye ni vema Mamlaka hizo zikumbuke kuwa, wale wananchi waliokuwa wakidanganywa kwa Pombe, Ubwabwa, Kanga, Skafu na vitu vingine, si wale wa 2015 wanaodai haki yao papo kwa papo, mtabanana mpaka kieleweke!
Si nia ya Makala hii kuwadharirisha Madiwani, Wabunge na Watendaji wa Rais, bali nawakumbusha ili mkumbuke kilichowaahidiwa kwa wananchi kuwa kinatakiwa kutekelezwa kabla ya wakati wa kuhojiwa kufika.
Nasema hivyo kwa sababu, wengi wenu bado wako usingizini, na wengine mko nje ya Majimbo yenu wala hamkumbuki kurudi na kushirikiana na wananchi! Nasema hivyo kwa maana moja tu kwamba, tangu mtoke Misiba, Majanga na Kero za watu wenu hamzijui, mnaenda tu mkisikia kwenye Luninga kuna matatizo.
Watu sasa wanataka Madiwani na Wabune wanaokaa nao Jimboni, kwenye Kata, ili kukitokea Janga si lazima watume taarifa Dar es Slaam au Ulaya waliko, bali waonje adha pamoja nao.
Hivyo Chonde, Rais, Wabunge na Madiwani, ili msije mkabubbujikwa na Machozi 2015, Nawataka timizeni ahadi zenu sasa! Maana watu waliziandika kwenye Mawe.
0715933308