Meneja wa Uwanja wa Shekhe Amri Abeid wa Arusha, David Joseph Mbaga akikoroga mbolea kwa ajili ya kuboresha nyasi za uwanja huo baada ya Bodi ya Ligi ya Soka Tanzania Bara kuufungia uwanja huo kutokana na kuwa katika hali mbaya. (Picha na Bryceson Mathias)
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid. unavyoonekana wakati ukiwa katika matengenezo.
Vijana wakiwa Jukwaa Kuu.
Uwanja wa Sheikh Amri Abeid. unavyoonekana wakati ukiwa katika matengenezo.
Vijana wakiwa Jukwaa Kuu.
Na Bryceson Mathias, Arusha
UONGOZI wa Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, umewalalamikia vijana wanaotumia mihadarati hususan bangi, vibaka na watoto wa mitaani (chokoraa), kwamba ndio wanaochangia kwa sehemu kubwa kuuchafua.
Uwanja huo maarufu, ambao hivi karibuni ulipigwa ‘stop’ na Bodi ya Ligi kutokana na kutokuwa katika hali nzuri, ambako ukipita ukutani na kwenye viti utakutana na michoro na harufu za haja kubwa na ndogo zikiwa zimezagaa.
Meneja wa Uwanja huo, David Mbaga ‘DJ’,
hasa baada ya kuona haja kubwa na ndogo zikitumika kuchora kuta, alisema, Uwanja huo kwa sehemu kubwa unachafuliwa na wavuta bangi, vibaka na chokoraa wanaoingia uwanjani hapo bila kudhibitiwa.
“Pamoja na kwamba wakiingia humu hujifanya wanaangalia wanamichezo wanaofanya mazoezi, lakini bila kutegemea, wao hujibanza pembezoni mwa kuta na badala ya kutumia vyoo wao hurundika haja zao kubwa na ndogo hapo hapo walipo, ambako mkishtuka wameshaondoka,” alisema na kuongeza.
Mimi nimeajiriwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM), kinachomiliki uwanja huu karibuni na sasa niko kwenye matazamio ndio maana unaona mimi na wadau wanaojitoa mali zao kama mbolea hii, tunashirikiana kuuboresha na kupanga mikakati ya kuwadhibiti waharibifu hawa.
Mbaga alisema, katika kuanza kudhibiti uharibifu huo, tayari wameshatengeneza milango yote minane iliyokuwa mibovu na kuwapa mwanya wahuni hao kujipenyeza kiholela uwanjani na sasa itakuwa inafungwa na kuwalazimu kupita alipo mlinzi.
Aidha, chokoraa na wanaosadikiwa wavuta bangi na vibaka waliokuwemo uwanjani hapo walipoulizwa, walikanusha na kudai wao ni watazamaji kama wengine na kuwepo kwao vikundi si kwamba ni wachafuzi, ila wanaweza kuwa walinzi wazuri kuliko inavyodhaniwa.
Hivi karibuni, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilitangaza kusaidia kuukarabati uwanja huo ili kuondoa dosari zilizopo, ili kuwezesha timu ya Taifa ya Bara, ‘Kilimanjaro Stars’ kuweka kambi jijini hapa ikijiwinda na michuano ya Chalenji, itakayopigwa jijini Nairobi .