Akizungumza
na wanahabari Jijini humo Mkuu wa Chaneli ya Sinema zetu Sophia Mgaza
amesema katika kutimiza msemo wao maarufu wa ‘burudani kwa wote’, Azam
TV vinara wa huduma bora za maudhui na burudani za kusisimua nchini, kwa
mara nyingine tena wanajivunia kutangaza uzinduzi wa tamthilia hizo
zilizokuwa zikisubiriwa kwa muda mrefu.
Amebainisha
kuwa tamthilia hizo zilizobeba simulizi za kuvutia si tu kwamba
zinakuja kuleta mapinduzi ya tasnia ya tamthilia nchini, bali zinaakisi
maisha halisi ya Watanzania wa rika zote na zinahusisha waigizaji wenye
vipaji na viwango vya juu.
“Uzalishaji
wa tamthilia hizi mbili Mtaa wa Kazamoyo na Lolita umezingatia mahitaji
ya soko kwani umetumia vifaa vya uzalishaji vya kisasa na ubora wa hali
ya juu wenye uwezo wa kutoa kazi katika viwango vya picha zenye ubora
na angavu yaani HD (High Definition). Lengo letu la kufanya mambo yote
haya ni kuendeleza dhamira yetu ya kutoa burudani ya hali ya juu kwa
watazamaji wetu”Amesema Sophia Mgaza.
Amesisitiza
kuwa Mtaa wa Kazamoyo na Lolita zimesanifiwa kwa uangalifu mkubwa ili
kuwapa watazamaji aina mbalimbali za simulizi za hadithi zenye kulinda
maadili ya Kitanzania, kutoa elimu kwa jamii na zinazotazamika na
familia yote na kutimiza majukumu yote matatu ya msingi yaani
kuhabarisha, kuburudisha na kuelimisha jamii.
Tamthiliya
ya Mtaa wa Kazamoyo na Lolita zimetayarishwa kwa ustadi mkubwa
zikishirikisha waigizaji mahiri, waandishi wenye ujuzi na watayarishaji
wazoefu na zinajumuisha viwango vya juu vya uzalishaji na mbinu za hali
ya juu ili kuhakikisha utazamaji wa kuvutia kwa hadhira.
Ameongeza
kuwa waanatarajia kuanza kupokea filamu hivi karibuni ambazo
wanategemea kupata hadithi zenye utafiti wakutosha, uhalisia wa
kitanzania na kugusa jamii ya kimataifa na hadithi zenye stori ndefu
isiyopungua dakika 90 na yenye viwango vya juu vya kimataifa inayoweza
kuchezwa kwenye majumba ya Sinema pamoja na bajeti yake.
Kwa
upande wake, Muandaaji wa Tamthilia ya Mtaa wa Kazamoyo, Mahsein
Awadhi (Dkt. Cheni) amesema tamthilia hiyo inasimulia hadithi inayohusu
maisha ya uswahilini na matukio wanayopitia wakazi wa Mtaa wa Kazamoyo.
Huu ni mtaa wenye sifa ya wanawake kukaa vibarazani na kupiga stori,
porojo pamoja na umbea huku vijana wa mtaa huu wakichagua maisha ya kuwa
vibaka ili kupata vipato kwa njia fupi na nyepesi kwao.
Katika
Mtaa huu viongozi wa Serikali ya Mtaa wanashindwa kudhibiti vitendo
hivyo na unaweza kusema wanafurahishwa na tabia za wakazi wake na ndio
maana wanakuwa mstari wa mbele kutetea maovu yanayoendelea dhidi ya
vyombo vya dola.
Katika
Mtaa wa Kazamoyo si ajabu kukuta watu wazima wakijihusisha kimapenzi na
vijana wadogo. Hii ni hadithi iliyojaa msisimko, migogoro na hadithi za
kuvutia kuhusu maisha halisi ya uswahilini.
“Tamthilia
hii imezalishwa na Kampuni ya Cheni Arts Creation Company Limited na
baadhi ya wasanii mashuhuri walioshiriki katika tamthilia hii ni pamoja
na Mahsein Awadhi (Dkt. Cheni), Amina Ahmed, Mwene Shina, Ester Darwesh,
Elizabeth Chijumba, Queen Masanja, Hashim Kambi, Abdallah Mkumbila
(Mzee Muhogo Mchungu), Pili Lway (Mama Nyamayao) Hajji Seif, Amini
Samofi, Karim Mandonga na wasanii wengine wengi waliopo katika tasnia na
wale wanaochipukia.” Amesema Dkt.Cheni.
Nae,
Muandaaji wa Tamthilia ya Lolita, William Mtitu amesema tamthilia hiyo
inatoa simulizi ya maisha ya vijana wa kisasa na namna wanavyokabiliana
na changamoto za kimahusiano yaliyojaa usaliti. Tamthilia hii pia inatoa
simulizi ya familia mbili zilizodhulumiana pesa na hivyo kila upande
ukiapa kulipiza kisasi kwa mwenzake, lakini kabla kisasi hakijakamilika
familia mojawapo inapata ajali ya ndege na kufariki dunia na hivyo
kumwacha binti yao kipenzi katika malezi ya familia hasimu ya wazazi
wake.
Familia
hiyo inaamua kudhulumu mali zote zilizoachwa na wazazi wa binti huyu
ambaye baadaye anakuja kupendana na mtoto wa kiume wa familia hii na
siku ya harusi yao anapata ajali mbaya ya gari na hivyo kumsababishia
ulemavu.
Ajali
hiyo imesababishwa na kijana aliyekuja kugundulika baadaye kuwa ni
ndugu yake wa damu. Baada ya ajali hii, siri nyingi zinaanza kugundulika
kuwa rafiki yake kipenzi ana uhusiano wa kimapenzi na mume wake, huku
mume wake naye akiwa na mpango wa kumdhulumu mali zote alizoachiwa na
baba yake. Kugundulika kwa siri hizi kunazua migogoro na hali ya
sintofahamu katika jamii inayowazunguka. Tamthilia hii imejengwa na
migogoro mingi ya kimapenzi baina ya marafiki, wazazi na vijana wadogo
na kati ya familia na familia. Ni simulizi ambayo unatakiwa kuiona
mwenyewe ili kuielewa vizuri.
“Tamthilia
hii imeandaliwa na Magazijuto Pictures chini ya muandaaji William
Mtitu. Miongoni mwa waigizaji mashuhuri katika tamthilia hii ni pamoja
na Angel Mazanda, Mariam Ismail, Christopher Mziwanda, Romeo George,
Genevieve Mpangala, Dennis David, Gysell Ngowi, Sadam Nawanda, Cojack
Chilo, Careen Simba, Jacqueline Materu, Neema Malita, Khalid Kuraish na
wasanii wengine wengi wanaofanya vizuri katika tasnia ya filamu
Tanzania” Amesema Bw. Mtitu.
Hata
hivyo tamthilia hizo zinachukua nafasi ya Fungu Langu itakayofikia
tamati tarehe 29 Julai 2023 na Jeraha itakayofikia tamati tarehe 10
Agosti, 2023 ambapo Burudani zote hizo zinapatikana kwa malipo ya
kifurushi cha Shilingi 8,000 kwa watumiaji wa kisimbuzi cha dishi na
antena.